Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambae ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM amesema hawezi kuifuta Jumuiya ya wazazi ya Chama hicho katika kipindi chake cha kuwa Mwenyekiti.
Jijini Dodoma Leo Rais Magufuli ameyasema hayo wakati anafungua mkutano wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM ambao ni mwendelezo wa mikutano ya uchaguzi wa Jumuiya mbalimbali za Chama hicho.
“Jumuiya hii ilianza mwaka 1955 ikiwa inaitwa Tanganyika African Parent Associations (TAPA), na aliyeianzisha ni Baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na anafahamu kwanini ilianza nikiifuta nitakuwa nimekosa busara na nitalaaniwa”, amesema Rais Magufuli.
Aidha Rais Magufuli ameongeza kuwa “Napenda niwahakikishie Jumuiya hii itaendelea kusimama kama zilivyo Jumuiya zingine ndani ya Chama”, ameongeza.
Aidha Rais magufuli amesifu mafanikio mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanywa na Jumuiya hiyo ikiwemo kumiliki shule mbalimbali pamoja na Chuo cha sanaa cha Kaole kilichopo Pwani. Mkutano huo unatarajiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wa taifa.
0 comments:
Post a Comment